1 Kings 18

Ilya Na Obadia

1 aBaada ya muda mrefu, katika mwaka wa tatu, neno la Bwana likamjia Ilya kusema, “Nenda ukajionyeshe kwa Ahabu na mimi nitanyesha mvua juu ya nchi.” 2 bKwa hiyo Ilya akaenda kujionyesha kwa Ahabu.

Wakati huu njaa ilikuwa kali sana katika Samaria,
3 cnaye Ahabu alikuwa amemwita Obadia ambaye alikuwa msimamizi wa jumba lake la kifalme. (Obadia alimcha Bwana sana. 4 dWakati Yezebeli alipokuwa akiwaua manabii wa Bwana, Obadia alikuwa amewachukua manabii mia moja na kuwaficha katika mapango mawili, hamsini kwenye kila moja na akawa akiwapa chakula na maji.) 5 eAhabu alikuwa amemwambia Obadia, “Nenda katika nchi yote kwenye vijito vyote na mabonde. Huenda tunaweza kupata majani ya kuwalisha farasi na nyumbu wapate kuishi ili tusilazimike kuwaua hata mmoja wa wanyama wetu.” 6Kwa hiyo wakagawanya nchi waliyokusudia kutafuta majani, Ahabu akaenda upande mmoja na Obadia upande mwingine.

7 fWakati Obadia alipokuwa akitembea njiani, Ilya akakutana naye. Obadia akamtambua, akamsujudia hadi nchi na kusema, “Je, hivi kweli ni wewe, bwana wangu Ilya?”

8Ilya akamjibu, “Ndiyo, nenda ukamwambie bwana wako Ahabu, ‘Ilya yuko hapa.’ ”

9Obadia akamuuliza, “Ni kosa gani nimefanya, hata ukaamua kumkabidhi mtumishi wako mkononi mwa Ahabu ili aniue? 10 gHakika kama Bwana Mwenyezi Mungu wako aishivyo, hakuna taifa hata moja au ufalme ambapo bwana wangu hajamtuma mtu kukutafuta. Kila wakati taifa au ufalme walipodai kwamba haupo huko, aliwafanya waape kwamba hawakuweza kukupata. 11Lakini sasa unaniambia niende kwa bwana wangu na kusema, ‘Ilya yuko hapa.’ 12 hSijui ni wapi Roho wa Bwana ataamua kukupeleka wakati nitakapokuacha. Kama nikienda kumwambia Ahabu na asikupate, ataniua. Hata hivyo mimi mtumishi wako nimemwabudu Bwana tangu ujana wangu. 13Je, hukusikia, bwana wangu, nilifanya nini wakati Yezebeli alipokuwa akiua manabii wa Bwana? Niliwaficha manabii wa Bwana mia moja katika mapango mawili, hamsini katika kila moja, nami nikawapatia chakula na maji. 14Nawe sasa unaniambia niende kwa bwana wangu na kumwambia, ‘Ilya yuko hapa.’ Yeye ataniua!”

15Ilya akasema, “Kama Bwana Mwenye Nguvu Zote aishivyo, yeye ninayemtumikia, hakika nitajionyesha kwa Ahabu leo.”

Ilya Juu Ya Mlima Karmeli

16Basi Obadia akaenda kukutana na Ahabu na kumwambia, naye Ahabu akaenda kukutana na Ilya. 17 iAhabu alipomwona Ilya, akamwambia, “Je, ni wewe, mtaabishaji wa Israeli?”

18 jIlya akamjibu, “Mimi sijaitaabisha Israeli. Lakini wewe na jamaa ya baba yako ndio mnaofanya hivyo. Mmeziacha amri za Bwana na mkafuata Mabaali. 19 kSasa waite watu kutoka Israeli yote tukutane nao juu ya Mlima Karmeli. Nawe uwalete hao manabii wa Baali mia nne na hamsini na hao manabii mia nne wa Ashera, walao chakula mezani mwa Yezebeli.”

20Ndipo Ahabu akatuma ujumbe katika Israeli yote na kuwakusanya manabii hao juu ya mlima Karmeli. 21 lIlya akasimama mbele ya watu na kusema, “Mtasitasita katika mawazo mawili hadi lini? Ikiwa Bwana ndiye Mungu, mfuateni yeye; lakini ikiwa Baali ni Mungu, basi mfuateni yeye.”

Lakini watu hawakusema kitu.

22 mKisha Ilya akawaambia, “Ni mimi peke yangu nabii wa Bwana aliyebaki, lakini Baali ana manabii mia nne na hamsini. 23Leteni mafahali wawili. Wao na wajichagulie mmoja, wamkate vipande vipande na waweke juu ya kuni lakini wasiiwashie moto. Nitamwandaa huyo fahali mwingine na kumweka juu ya kuni lakini sitawasha moto. 24 nKisha mliitie jina la mungu wenu, nami nitaliitia jina la Bwana Mwenyezi Mungu yule ambaye atajibu kwa moto, huyo ndiye Mungu.”

Kisha watu wote wakasema, “Hilo unalosema ni jema.”

25Ilya akawaambia manabii wa Baali, “Chagueni mmoja kati ya hawa mafahali na mwe wa kwanza kumwandaa, kwa kuwa ninyi mko wengi sana. Liitieni jina la mungu wenu, lakini msiwashe moto.” 26 oKwa hiyo wakamchukua yule fahali waliyepewa, nao wakamwandaa.

Kisha wakaliitia jina la Baali kutoka asubuhi hadi adhuhuri, wakapiga kelele, “Ee Baali, utujibu!” Lakini hapakuwa na jibu; hakuna aliyejibu. Nao wakacheza kuizunguka madhabahu waliyoijenga.

27Wakati wa adhuhuri, Ilya akaanza kuwadhihaki, akisema, “Pigeni kelele zaidi! Hakika yeye ni mungu! Labda amezama katika mawazo mazito, au ana shughuli nyingi, au amesafiri. Labda amelala usingizi mzito, naye ni lazima aamshwe.” 28 pKwa hiyo wakapiga kelele zaidi na kama ilivyokuwa desturi yao wakajichanja wenyewe kwa visu na vyembe, mpaka damu ikachuruzika. 29Adhuhuri ikapita, nao wakaendelea na utabiri wao wa kiwazimu mpaka wakati wa dhabihu ya jioni. Lakini hapakuwa na jibu, hakuna aliyejibu, hakuna aliyeangalia.

30 qKisha Ilya akawaambia watu wote, “Sogeeni karibu nami.” Watu wote wakamkaribia, naye akakarabati madhabahu ya Bwana, ambayo ilikuwa imevunjwa. 31 rIlya akachukua mawe kumi na mawili, moja kwa ajili ya kila kabila la wana wa Yakobo, ambaye neno la Bwana lilimjia, likisema, “Jina lako litakuwa Israeli.” 32 sKwa mawe hayo, akajenga madhabahu katika jina la Bwana, na akachimba handaki kuizunguka, ukubwa wa kutosha vipimo viwili vya mbegu. 33 tAkapanga kuni, akamkata yule fahali vipande vipande na kuvipanga juu ya kuni. Kisha akawaambia, “Jazeni mapipa manne maji na kuyamwaga juu ya sadaka ya kuteketezwa na juu ya kuni.”

34Akawaambia, “Fanyeni hivyo tena.” Nao wakafanya hivyo tena.

Akaagiza, “Fanyeni kwa mara ya tatu.” Nao wakafanya hivyo kwa mara ya tatu.
35Maji yakatiririka kuizunguka madhabahu na hata kujaza lile handaki.

36 uWakati wa kutoa dhabihu ya jioni, nabii Ilya akasogea mbele na kuomba, akisema: “Ee Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na Isaka na Israeli, ijulikane leo kwamba wewe ndiye Mungu katika Israeli na ya kwamba mimi ni mtumishi wako na nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. 37Unijibu mimi, Ee Bwana, nijibu mimi, ili watu hawa wajue kwamba wewe, Ee Bwana, ndiwe Mungu, na kwamba unaigeuza mioyo yao ikurudie tena.”

38 vKisha moto wa Bwana ukashuka na kuiteketeza ile dhabihu, zile kuni, yale mawe, ule udongo, na pia kuramba yale maji yaliyokuwa ndani ya handaki.

39Wakati watu wote walipoona hili, wakaanguka kifudifudi na kulia, “Bwana: yeye ndiye Mungu! Bwana: yeye ndiye Mungu!”

40 wKisha Ilya akawaamuru, “Wakamateni hao manabii wa Baali. Msimwache hata mmoja atoroke!” Wakawakamata, naye Ilya akawaleta mpaka Bonde la Kishoni na kuwachinja huko.

41Ilya akamwambia Ahabu, “Nenda, ukale na kunywa, kwa kuwa kuna sauti ya mvua kubwa.” 42 xHivyo Ahabu akaondoka ili kula na kunywa. Lakini Ilya akapanda kileleni mwa Karmeli, akasujudu na akaweka kichwa chake katikati ya magoti yake.

43Akamwambia mtumishi wake, “Nenda ukatazame kuelekea bahari.” Akaenda na kutazama.

Akasema, “Hakuna kitu chochote huko.”

Mara saba Ilya akasema, “Nenda tena.”

44 yMara ya saba, mtumishi akaleta taarifa, “Wingu dogo kama mkono wa mwanadamu linainuka kutoka baharini.”

Hivyo Ilya akasema, “Nenda ukamwambie Ahabu, ‘Tandika gari lako na ushuke kabla mvua haijakuzuia.’ ”

45 zWakati ule ule anga likawa jeusi kwa mawingu, upepo ukainuka na mvua kubwa ikanyesha, naye Ahabu akaenda zake Yezreeli. 46 aaNguvu za Bwana zikamjia Ilya, naye akajikaza viuno, akakimbia mbele ya Ahabu njia yote hadi maingilio ya Yezreeli.
Copyright information for SwhKC